Na Mussa Juma, Mwananchi
Arusha. Wakati
joto la urais likizidi kupanda ndani ya CCM kutokana na hofu ya baadhi
ya majina mazito ya wagombea wa nafasi hiyo kukatwa kwa mizengwe, vita
vya wagombea sasa ni dhahiri baada ya mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM kusema
hakuna mtu atakayekatwa bila ya sababu za msingi.
Mjumbe huyo, Sadifa Juma Hamisi, ambaye ni mwenyekiti wa Umoja wa Vijana
wa CCM (UVCCM), pia alisema umoja huo haujafikia uamuzi wala kumtuma
mtu kumdhibiti mwanachama anayetajwa kuwania urais.
Katika siku za karibuni kumekuwapo mjadala mkubwa ndani ya CCM juu ya
mtu atakayepitishwa kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho, na ilizidi
baada ya Rais Jakaya Kikwete kueleza kuwa mwanachama ambaye atateuliwa
na CCM kugombea urais hayumo miongoni mwa waliojitokeza na kuwataka
wanachama kuwashawishi watu wenye sifa wajitokeze.
Siku chache baadaye, Dk Raphael Chegeni aliliambia gazeti la Mwananchi
kuwa ametumwa na wanachama wa CCM wa mikoa ya Kanda ya Ziwa kwenda
kumshawishi Lowassa kujitokeza kuwania urais kuitikia wito wa Rais
Kikwete wa kuwataka wanachama kuwashawishi watu wenye sifa kujitokeza.
Hadi sasa, wanachama waliojitokeza kuwania kuteuliwa na CCM kugombea
urais ni Waziri Mkuu Mizengo Pinda, January Makamba (Naibu Waziri wa
Sayansi na Teknolojia), Hamisi Kigwangala, na Lazaro Nyalandu ambaye ni
waziri wa Maliasili na Utalii.
Lakini pia wako wanaotajwa kuwania urais lakini hawajatangaza ambao ni
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sita, William Ngeleja,
Emmanuel Nchimbi, Mwigulu Nchemba, Stephen Wasira, Bernard Membe na
Edward Lowassa ambaye ameibua mjadala kati ya kambi yake na
zinazompinga.
Mapema wiki iliyopita, katibu wa uhamasishaji na chipukizi wa UVCCM,
Paul Makonda alikaririwa akisema kuwa vitendo vyake vya kumshambulia
Lowassa vinatokana na kutumwa na umoja huo kumdhibiti, jambo ambalo
limezidisha mjadala kuhusu mteule wa chama hicho.
Kutokana na hofu hiyo, viongozi wa UVCCM na CCM mkoani Arusha wametuma
ujumbe wa maneno kwa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa za chama
hicho wakitaka wanachama wasifanyiwe kile wanachokiita kuchafuana na
vitisho vya baadhi ya wagombea kukatwa kimizengwe.
Ujumbe huo ulitumwa juzi na mwenyekiti wa CCM wa mkoa, Onesmo ole
Nangole na mwenyekiti wa UVCCM, Robinson Meitinyiku ambao walitaka
Sadifa Juma Hamis kueleza msimamo wa mkoa kwa vyombo hivyo viwili vya
maamuzi, na mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya CCM aliwahakikishia kuwa hakuna
mgombea atakayekatwa kwa “sababu za kijinga”.
Akijibu ujumbe wa viongozi hao, Sadifa aliyekuwa jijini hapa kumsimika
kamanda wa vijana wa wilaya ya Arumeru, Mathias Manga, aliwaondolea hofu
katika hafla hiyo akisema hakuna mgombea wa urais wa CCM ambaye
atakatwa bila sababu za msingi, lakini akawataka vijana kusubiri zamu
yao hadi 2025.
Kauli ya Sadifa
“Niwaombeni mwenyekiti wa mkoa na mwenyekiti wa UVCCM, msiogope. Hakuna
mtu atakayekatwa kijinga ndani ya Kamati Kuu au Halmashauri Kuu. Kikubwa
tufuate maadili. Mimi mchapakazi ndiye nitamtetea,” alisema bila kutaja
mgombea anayekusudiwa.Alisema
ni lazima kiongozi bora awe na mikakati na dira na upeo wa kuwa na
mikakati bora ya kutekeleza ahadi zake kwani hatuwezi kuwa na kiongozi
ambaye hana dira wala mikakati.
“Tunataka kiongozi mwenye kujiamini, awe ana vision (dira) na mission
(mikakati), msikivu... hatuwezi kuchagua rais ambaye hana sifa hizi,”
alisema.
Akizungumzia maombi ya Nangole kuhusu tabia ya kuwachafua baadhi ya
wagombea na kuwatisha, Sadifa alisema hakuna kiongozi aliyetumwa na CCM
na UVCCM kutukana mtu wala kumtisha.
“Mzee wangu, watu wengi wanajua wanamtaka nani, ukiona mtu anapanda
kwenye majukwaa anamchafua mwenzake, ujue huyo ana mapungufu ya malezi,
hakuna haja ya kumjibu kwani utaonekana na pia wewe una mapungufu,”
alisema.
Akionekana kujibu kauli ya Makonda, Sadifa alisema UVCCM haijatuma mtu
amtukane mwingine. Alisema akiwa mjumbe wa Kamati Kuu, hawajawahi
kumtuma kiongozi yoyote kumtukana mwanachama mwingine wa CCM.
Alipoulizwa kuhusu hofu hiyo, kwa kifupi katibu wa itikadi na uenezi wa
CCM, Nape Nnauye alisema: “Mimi siwezi kuwa msemaji wa Umoja wa Vijana,
nikisema niwajibu nitakuwa nimepotoka.”
Mapema wiki iliyopita, Makonda alikaririwa akisema kuwa amekuwa
akimshambulia Lowassa, ambaye anatajwa kuwania urais kupitia CCM, kwa
sababu ametumwa na umoja huo.
Makonda amekuwa akikaririwa mara kwa mara akisema kuwa Lowassa hafai
kuwa mteule wa CCM wa kuwania urais na mikanda ya kauli zake imesambaa
kwenye mitandao ya kijamii, jambo lililofanya uteuzi wake kuwa Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni uhojiwe na watu wengi na hivyo kujikuta akilazimika
kusema ametumwa na umoja wake kumdhibiti waziri mkuu huyo wa zamani.
Katika mazungumzo yake juzi, Sadifa hakutaka kutaja jina la mgombea
atakayemtetea wala mtu anayemshambulia, badala yake alisema muda
ukifika, kila kitu kitajulikana kwa kuwa watu wanamjua mgombea
wanayemtaka.
“Mwenyekiti, dawa ya mjinga ni kukaa kimya, watu wanamjua mtu ambaye
wanamtaka. Rais Jakaya Kikwete ni mtu ambaye hatabiriki, hana
ushemeji... nyie subirini tu wakati ukifika,” alisema.
Vijana na urais
Akizungumzia vijana ambao wanautaka urais, Sadifa aliwataka kusubiri zamu yao hadi 2025 ili wazee waliopo wamalize muda wao.
Alisema utakapofika mwaka 2025 vijana watakuwa katika nafasi nzuri sana
ya kushika uongozi na hawatakubali kuona viongozi wazee wakitaka kupewa
nafasi.
“Wazee tutawaomba radhi mwaka wenu ni 2015 hadi 25, mkimaliza hapo, miaka yenu imekwisha, msije tena,” alisema.
Kauli ya Nangole
Awali, Nangole, ambaye aliwahi kusema kuwa Lowassa ni kiongozi msikivu
na makini na ambaye ni tegemeo la Watanzania katika kuwaunganisha kuwa
kitu kimoja, aliomba Kamati Kuu ipelekewe ujumbe kuwa CCM mkoani Arusha
hairidhishwi na matendo ya baadhi ya viongozi kuwatukana na kuwatisha
wengine.
Nangole alirejea kauli aliyowahi kuitoa kuwa CCM ni ya wanachama wote na
ndani yake hakuna sisimizi au tembo wa kumtisha mwingine ili mradi
anafuata taratibu za chama hicho.
Alisema imeibuka tabia ya baadhi ya viongozi wa CCM, kuwatisha wengine
na kuwatukana kana kwamba wao ndio wana hatimiliki ya CCM.
Naye mwenyekiti wa UVCCM mkoani Arusha, Robinson Meitinyiku alisema kuna
kiongozi mmoja ametoa kauli kuwa mgombea mmoja hata kama akisafishwa na
madodoki hawezi kuwa msafi.
Badala yake alisema kiongozi aliyetoa maneno hayo ndiye hawezi
kusafishika hata kwa gunzi kwani kuna taarifa aliwahi kusaliti na
kujiunga na chama kingine.
No comments:
Post a Comment