Ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia (WB) inaonesha kuwa, nchi ya
Tanzania haiko tena katika kundi la nchi 10 masikini zaidi duniani. Kwa
mujibu wa Benki ya Dunia, ripoti hiyo imezingatia pato la taifa, ambalo
kimsingi huwa ni jumla ya thamani ya bidhaa zilizozalishwa kwa kipindi
fulani, mara nyingi kwa mwaka, kikigawanywa kwa idadi ya watu ndani ya
nchi husika. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi 10 maskini zaidi duniani ni
Malawi, ambayo pato la kila mwananchi wa taifa hilo kwa mwaka, ni dola
za Kimarekani 226.50. Malawi inafuatiwa na Burundi, Dola 267.10, Jamhuri
ya Afrika ya Kati (CAR), Dola 333.20, Niger, Dola 415.40, Liberia, Dola
454. 30 na Madagascar, Dola 463. Aidha mataifa mengine na pato la kila
mwananchi, ni ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Dola 484.20,
Gambia, Dola 488.60, Ethiopia, Dola 505, na nchi ya 10 kwa umaskini ni
Guinea, ambako pato la mwananchi ni Dola 523.10. Akizungumzia sababu
zilizochangia Tanzania kuondoka kwenye kundi hilo la nchi 10 maskini
zaidi duniani, Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam,
Profesa Haji Semboja amesema kuwa, hilo linaonyesha kuwa Tanzania
imeweza kujenga uwezo wa kuzimiliki, kuzisimamia, na kuziendesha
rasilimali nyingi ilizojaaliwa, ili kuboresha ustawi wa wananchi na
taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment